Jumatano, Januari 8, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 7 Rajab 1446 Hijria sawa na 8 Januari 2025
Miaka 383 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78.
Alizaliwa katika mji wa Pisa na kusoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua.
Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya Abu Raihan Biruni, msomi mashuhuri wa Iran, ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, yaani tarehe 8 Januari mwaka 1932 ulianza utawala wa kifalme wa Abdul-Aziz Ibn Saud katika eneo la Bara Arabu kupitia msaada wa Uingereza.
Abdul-Aziz Ibn Saud, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa makabila ya Hijaz, alianzisha mapigano dhidi ya utawala wa Othmania mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 na kupata ushindi. Mwaka 1903 mtawala wa Kiothmania alitimuliwa katika eneo la ya al-Ahsa huko Hijazi na tukio hilo lilikuwa jiwe la msingi wa kuasisiwa utawala wa Aal-Saud katika maeneo hayo. Katika kipindi cga Vita vya Kwanza vya Dunia, Aal-Saud waliingia ubia wa urafiki na Uingereza. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo vilivyomalizika kwa kushindwa vibaya utawala wa Othomania, utawala huo ulifikia tamati kikamilifu katika eneo hilo la Bara Arabu. Katika vita vilivyopiganwa baina ya Abdul-Aziz Ibn Saud na mtawala Hussein Bin Ali Sharif aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, Ibn Saud aliibuka mshindi na akatwaa kwa nguvu eneo hilo la Hijaz.
Hatimaye mwaka 1926 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Uingereza na mtawala huyo huyo wa Kiwahabi, Abdul-Aziz Ibn Saud alijitangaza kuwa kiongozi wa Hijaz. Mwaka 1927 Ibn Saud alijitangaza rasmi kuwa mtawala wa Hijaz na Najd na tarehe 8 Januari mwaka 1932 Abdul Aziz alitangazwa kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Hadi kutwaa madaraka ya eneo lote la Hijaz, watu wa kizazi cha Aal Saudi walifanya mauaji mengi na umwagaji damu mkubwa na kuwalazimisha watu wa maeneo hayo kufuata fikra na itikadi potufu za kiwahabi.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, maandamano makubwa ya kwanza ya wananchi Waislamu wa Iran baada ya Harakati ya 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia yalifanyika mjini Qum hapa nchini dhidi ya utawala wa Shah.
Maandamano hayo yalifanyika baada ya gazeti moja la alasiri kuchapisha makala iliyomvunjia heshima Imam Ruhullah Khomeini.
Katika maandamano hayo wananchi na wanazuoni wa mji wa Qum walikusanyika katika Msikiti Mkuu wa mji huo na kutaka kuondolewa madarakani utawala wa Shah. Jeshi la Shah lilishambulia waandamanaji na kuua wengi miongoni mwao.
Baada ya tukio hilo wanazuoni wengi wa Kiislamu walipelekwa uhamishoni katika miji mbalimbali ya Iran na tarehe 19 Dei 1356 ilitambuliwa kuwa mwanzo wa kupamba moto harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita aliga dunia Ayatullah Ali Akbar Hashemi Bahremani maarufu kwa jina la Ali Akbar Hashemi Rafsanjani akiwa na umri wa miaka 82 kutokana na matatizo ya moyo.
Ayatullah Rafsanjani anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri sana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alizaliwa katika kijiji cha Bahreman huko Rafsanjani katika familia tajiri kiasi na kupata elimu ya dini katika mji mtakatifu wa Qum. Huko alijiunga na wanaharakati waliokuwa wakipinga utawala wa dhalimu wa Shah waliokuwa wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini.
Ayatullah Rafsanjani alikamatwa na kufungwa jela mara kadhaa na utawala wa Shah. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Rafsanjani alishika nyadhifa nyingi ikiwemo ya uspika wa Bunge, Rais wa jamhuri na mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.
