Iran yaghariki katika furaha na sherehe ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw)
Iran ya Kiislamu inasherehekea tukio adhimu na la kipeee la siku ya kupewa Utume Nabii Muhammad bin Abdullah (saw).
Sherehe za kukumbuka tukio hilo adhimu katika historia ya mwanadamu zilianza jana jioni kote hapa nchini katika usiku wa kuamkia tarehe 27 mwezi wa Rajab.
Sherehe na tafrija ziliaanza kuonekana katika maeneo yote ya vijijini na mijini hususan katika miji mitakatifu ya Mash'had na Qum ambako waumini wanakusanyika kusherehekea siku ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad Mwaminifu, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake. Sherehe hizo zinaendelea leo kote nchini na siku hii ya tarehe 27 Rajab, siku ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw) ni likizo ya kitaifa nchini Iran.
Kwa mujibu wa historia na mafundisho ya Uislamu, Mtume Muhammad (saw) alipewa utume katika siku kama ya leo tarehe 27 Rajab, miaka 13 kabla ya hijra na kuhamia Madina.
Kabla ya kupewa utume, Muhammad alikuwa maarufu katika jamii ya Makkah kwa kusema ukweli, uaminifu na kutenda mema. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa.
Idhaa ya Kiswahili ya Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa siku hii adhimu.