Iran yakataa masharti ya Marekani kwenye mazungumzo ya nyuklia
Iran imesisitiza haitakubali kamwe masharti yoyote ya kusitisha urutubishaji wa urani, ikisema mafanikio yake ya nyuklia ni matokeo ya miaka mingi ya kujitolea, uwekezaji, na kujenga uwezo wa kitaifa.
Kupitia ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesisitiza kuwa urutubishaji wa urani ni haki ya Iran isiyoweza kujadiliwa katika makubaliano yoyote ya baadaye kuhusu mpango wa nyuklia.
"Kuna sababu kwanini ni mataifa machache tu ulimwenguni yanayoweza kutoa nishati ya kuendesha mitambo ya nyuklia," aliandika. "Iran imelipa gharama kubwa kufikia uwezo huo, na hakuna hali yoyote ambayo tunaweza kuwasaliti wazalendo waliotimiza ndoto hii ya taifa."
Araghchi amesema kuwa urutubishaji wa urani ni zao la dhamira ya kifedha ya Iran, misingi imara ya viwanda, pamoja na miundombinu ya kielimu na kiteknolojia ; mambo msingi yaliyoiwezesha Tehran kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani licha ya miaka mingi ya vikwazo na mashinikizo ya kimataifa.
Akitolea ufafanuzi msimamo wa Iran katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani, Araghchi amesema bayana kuwa:
"Hakuna utajirishaji, basi hakuna makubaliano." Aidha amesema: "Hakuna silaha za nyuklia. Hapo tunaweza kuwa na makubaliano."
Iran na Marekani tayari zimefanya duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ili kutafuta njia mbadala ya Mkataba wa Nyuklia wa 2015 (maarufu kama JCPOA).
Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekwama kutokana na shinikizo la Marekani kwamba Iran iache kabisa utajirishaji wa urani chini ya mkataba wowote mpya, sharti ambalo Tehran imelipinga vikali.
Maafisa wa Iran wameweka wazi kuwa hawatakubali kupokonywa haki yao ya msingi katika sekta ya nyuklia, wakisisitiza kuwa shughuli zao hazilengi utengenezaji wa silaha za nyuklia, bali ni kwa matumizi ya kiraia na maendeleo ya kitaifa.