WHO: Inawezekana kuitokomeza Ebola ndani ya miezi 3
-
WHO: Tunaweza kudhibiti kasi ya Ebola
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa bado kuna uwezekano wa kudhibiti mlipuko wa Ebola ambao unaenea kwa kasi inayopiku juhudi za kuuzuia, na ambao umekuwa mlipuko wa pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa.
Hayo yamesemwa na Thierno Balde, Mkurugenzi wa Masuala ya Dharura wa WHO, akiwahutubia waandishi wa habari mjini Geneva jana Jumanne, akizungumza kutokea Bunia, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kueleza kuwa: "Kuhusu mpango unaofuata wa miezi mitatu, ndiyo, iwapo rasilimali zinazohitajika zipo, nadhani itawezekana kufanya hivyo."
Ameongeza kuwa, kwa sasa, rasilimali zilizopo hazikidhi mahitaji, na WHO imefanikiwa kupata takriban asilimia 60 tu ya dola milioni 115 inazohitaji kwa ajili ya kukabiliana na Ebola. Changamoto nyingine ni pamoja na kuchelewa kugundua maambukizi, timu za ufuatiliaji kuzidiwa na kazi, migogoro ya kivita, pamoja na ukosefu wa chanjo na tiba kwa ajili ya aina adimu ya virusi hivyo inayojulikana kama Bundibugyo.
Shirika hilo la kimataifa la afya lilisema mapema mwezi huu kuwa, inawezekana kuzuia na kudhibiti kasi ya kuenea kwa Ebola ndani ya kipindi cha miezi mitatu, lakini tangu wakati huo kumekuwa na dalili kwamba hali imezidi kuwa mbaya, huku ugonjwa huo ukisambaa hadi katika mkoa wa sita.
Mlipuko huu ambao ni mbaya zaidi kati ya milipuko 17 iliyowahi kutokea nchini Kongo DR, umesababisha vifo vya watu wasiopungua 2,325 hadi sasa.