Mufti wa Oman ataka mataifa ya dunia kujifunza kutoka kwa Yemen
(last modified Thu, 05 Jun 2025 12:53:15 GMT )
Jun 05, 2025 12:53 UTC
  • Mufti wa Oman ataka mataifa ya dunia kujifunza kutoka kwa Yemen

Mufti Mkuu Oman, Sheikh Ahmed bin Hamad Al-Khalili, amesisitiza kuwa, leo hii majeshi ya madola dhalimu na ya kibeberu duniani yameinamisha vichwa vyao mbele ya Yemen na ameyataka mataifa yanayotaka kuwa huru duniani, kuiga mfano wa Yemen katika kukabiliana na maadui wa mataifa yao.

Sheikh Al-Khalili amesema hayo katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa "X" na huku akizungumzia vita vya vikosi vya Yemen na Marekani katika Bahari ya Shamu (Bahari Nyekundu) ameandika: "Kuna mafunzo na maadili makubwa tuliyoyaona… Mambo ya kufurahisha tuliyoyashuhudia huko Yemen ni mengi… linatutosha somo tulilopata kutokana na kusimamia kwao imara kukabiliana na dola kubwa la dhulma na na la kibeberu (Marekani) na kulilazimisha kusalimu amri na kurudi nyuma. Rais wa dola hilo, (Trump), anajulikana kwa kiburi na majivuno, lakini mwishowe alimwomba Sultani wa Oman, mwanzilishi wa amani na mtetezi wa mageuzi, kupatanisha (baina ya Marekani) na makomandoo mashujaa wa Yemeni ili kufikia mapamtano na amani.”

Aidha ameandika: "Na sasa tunasikia kwamba Uingereza imewaomba makomandoo hao mashujaa (wa Yemen) kuruhusu meli yake kupita kwenye Lango-Bahari la Bab al-Mandab. Waliiwekea masharti (Uingereza) na ilikubali kwa utii kamili," akimaanisha ombi la Uingereza kwa Yemen la kuiruhusu manuwari yake ya kubeba ya ndege, HMS Prince of Wales, kupita katika Bahari Nyekundu.

Mufti wa Oman, Sheikh Al-Khalili ametoa mwito kwa tawala za Kiarabu zinazoyanyenyekea madola ya kibeberu kupata somo na kuiga mfano wa Yemen. Amesema: “Kwanza, wale waliochukua maamuzi ya kunyenyekea na kusujudu (mbele ya madola ya kiistikbari) wanapaswa kuzingatia jambo hili, kwani hilo linawazidishia unyonge,” akatoa mfano wa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Je, wanatafuta utukufu kwao? (An-Nisaa 139).

Mufti Mkuu wa Oman ametamatisha ujumbe wake muhimu kwa kusema: “Watu wenye hikma wanapaswa kuzingatia jinsi taifa hili (la Yemen) lilivyo leo. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema kweli: “Hakika Mwenyezi Mungu habadili hali za watu mpaka wabadili yaliyomo nafsini mwao.” (Ar-Ra’d 11).