Rouhani: Iran na Uturuki ni nanga ya utulivu katika eneo hili
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi mbili za Iran na Uturuki ni rafiki na zenye nguvu katika eneo hili na kwamba Iran na Uturuki ni nanga ya utulivu katika eneo nyeti la Mashariki ya Kati.
Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari hapa Tehran akiwa na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyep Erdogan, Dakta Hassan Rouhani ameeleza kuwa lengo la mwisho la nchi mbili hizi ni kurejesha amani, utulivu na usalama katika eneo hili.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mgogoro wa Syria na jitihada zisizo za kisheria za viongozi wa Kurdistan ya Iraq za kutaka kujitenga na nchi hiyo na kubainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki hazitakubali kutokea mabadiliko yoyote katika mipaka ya kijiografia ya eneo hili. Rais Rouhani amesema, Iran na Uturuki wanaamini kuwa hatua ya kutaka kujitenga na kushadidi hitilafu za kikaumu na kimadhehebu katika Mashariki ya Kati ni matokeo ya njama zinazofanywa na nchi ajinabi na kwamba kwa mtazamo wa nchi mbili hizi, ardhi za nchi za Iraq na Syria zinapasa kubaki kuwa moja.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia uhusiano wa Iran na Uturuki na kueleza kuwa serikali hizo mbili zina azma ya kuboresha mahusiano yao katika nyanja zote. Dakta Rouhani amesema, mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Uturuki yatafikia dola milioni 30 kwa mwaka.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Rais wa Uturuki ameashiria msimamo wa pamoja kati ya Iran na Uturuki kuhusu kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo la Kurdistan huko Iraq na kubainisha kuwa Uturuki na Iran zinaitambua kura hiyo ya maoni kuwa kinyume cha sheria.