Sherehe za Nairuzi katika Umoja wa Mataifa
(last modified Tue, 22 Mar 2016 07:02:06 GMT )
Mar 22, 2016 07:02 UTC
  • Sherehe za Nairuzi katika Umoja wa Mataifa

Sherehe za kuadhimisha siku kuu ya Nairuzi (Nowruz) zimefanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa umoja huo.

Ghulam-Ali Khoshroo, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amehutubia sherehe hiyo na kusema: "Nairuzi ni tukio la kiutamaduni na kijamii na ambalo linaakisi furaha, kuwa pamoja watu, kutunza mazingira, wastani wa mambo, usafi wa nyumba na mtu binafsi mbali na kuwa na ujumbe wa matumaini, furaha, nuru, maisha bora na mapenzi."

Khoshroo ameongeza kuwa, katika dunia ambayo misimamo mikali inaenea sambamba na ugaidi, vita na mauaji, Nairuzi inaleta ujumbe wa usalama na kuelewana wanadamu. Ameongeza kuwa Nairuzi ni fursa nzuri kwa jamii ya mwanadamu kuangazia uzuri wa urafiki, amani na kushirikiana watu wa dunia. Akihutubia sherehe hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametuma salamu za kheri na fanaka kwa watu wa Iran na nchi zote zinazoadhimisha Nairuzi ambayo ni mwanzo wa msimu wa machipuo.

Akiashiria migogoro ya kieneo na duniani, Ban amesema Nairuzi ni fursa nzuri sana ya kuonyesha azma imara ya kujenga mustakabali bora na kuleta amani endelevu.

Ikumbukwe kuwa Mwaka 2009 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni UNESCO lilitangaza na kuisajili Nairuzi kama turathi ya kimaanawi duniani. Aidha Mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin yaani Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nairuzi. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nairuzi kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, siku kuu ya Nairuzi hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa wa urafiki baina ya watu wa jamii mbali mbali.