Iran yapendekeza kuundwa kambi tofauti za kiuchumi katika nchi za Kiislamu
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuundwa kambi tofauti za kiuchumi katika nchi za Kiislamu kulingana na uwezo wa nchi husika kwa shabaha ya kupanua hisa ya nchi hizo katika uchumi wa kimataifa ni jambo la dharura.
Muhammad-Javad Azari Jahromi amesema hayo nchini Malaysia katika mkutano wa 13 wa Baraza la Kimataifa la Uchumi wa Kiislamu (WIFE) na kupendekeza suala la kufanyika utafiti juu ya uwezekano wa kuanzisha kambi mbalimbali za kiuchumi miongoni mwa nchi za Kiislamu kwa kuzingatia utaalamu, vyanzo na maliasili zilizoko katika nchi husika ili Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Benki ya Ustawi wa Kiislamu (IDB) ziweze kuainisha Ramani ya Njia.
Muhammad-Javad Azari Jahromi ametangaza utayari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuchangia katika kufanya utafiti huo na kuongeza kuwa, kuanzishwa kambi kadhaa katika nchi za Kiislamu kunaweza kutoa huduma zaidi kwa nchi zote za Kiislamu.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, bila ya kuweko ushindani hakuwezi kuweko tuzo kwa waletaji mambo mapya, hivyo nchi za Kiislamu zinapaswa kujiandaa kwa ushindani na pia zijilinganishe na ulimwengu ili kwa njia hiyo ziweze kuendelea na maisha yao kwa upande wa uchumi.
Muhammad-Javad Azari Jahromi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumatatu ya juzi aliwasili Kuala Lumpur mji mkuu wa Malysia kwa shabaha ya kushiriki katika Mkutano wa Baraza Kimataifa la Uchumi wa Kiislamu.