Rais Rouhani apongeza umoja wa kidini nchini Iran
(last modified Sun, 03 Jun 2018 08:07:00 GMT )
Jun 03, 2018 08:07 UTC
  • Rais Rouhani apongeza umoja wa kidini nchini Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza umoja miongoni mwa dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini akisisitiza kuwa serikali yake imeazimia kulinda haki za jamii zote.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumamosi katika mkutano na kundi la wanazuoni wa Kisunni hapa mjini Tehran na kufafanua kuwa, madhehebu za Shia na Sunni zinatofautiana katika masuala madogo madogo lakini zina thamani nyingi za kufanana.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, licha ya umoja na mshikamano wa Waislamu wa Iran pasina kujali tofauti zao za kimadhahebu, au kuheshimiwa haki za dini zenye wafuasi wachache, lakini nchi ajinabi zingali zinashadidisha mashinikizo dhidi ya taifa la Iran.

Rais Rouhani ameyasema hayo siku chache baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kudai katika ripoti yake ya uhuru wa kidini ya mwaka 2017 ambayo ilitolewa Jumanne iliyopita kuwa, eti hakuna uhuru wa kidini nchini Iran.

Kanisa la Kikatoliki mjini Tehran

Akitoa radimali yake kuhusu ripoti hiyo, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema ripoti hiyo haikuzingatia ukweli wa mambo, haina mashiko wala msingi wowote bali imetolewa kwa malengo ya kiuadui na kwa shabaha ya kutumia vibaya dini kwa malengo ya kisiasa.

Naye Askofu Mkuu wa Wakristo wa Kiarmenia wa Tehran na kaskazini mwa Iran alisema wafuasi wa dini za Mwenyezi Mungu, iwe ni Waislamu wa Kisuni na Kishia au Wakristo wa Orthodox na Protestant na wafuasi wa dini nyingine, wanaishi pamoja kwa usalama na amani chini ya kivuli cha Jamhuri ya Kiislamu na wanapata haki zao zote za kiraia kwa usawa bila ya unyanyasaji wala ukandamizaji wa aina yoyote ile.