Iran yailalamikia Ufaransa kwa kuwahami na kuwafadhili magaidi wa MKO
(last modified Thu, 21 Jun 2018 03:11:28 GMT )
Jun 21, 2018 03:11 UTC
  • Iran yailalamikia Ufaransa kwa kuwahami na kuwafadhili magaidi wa MKO

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa ameilalamikia serikali ya Ufaransa kwa kuwafadhili, kuwahami na kuwaruhusu magaidi wa MKO kufanya shughuli zao nchini humo licha ya magaidi hao kuwa na historia chafu ya kufanya ugaidi ndani na nje ya Iran.

Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana (Jumatano) katika duru ya tano ya mazungumzo ya kisiasa baina ya Iran na Ufaransa hapa Tehran. Amesema hayo wakati alipokutana na Gordo Montaigne, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa na kuitaka Paris ilipige marufuku genge la kigaidi la MKO kufanya shughuli zake nchini humo.

Kwa upande wake, katibu mkuu huyo wa Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa amesema, nchi yake inafuatilia kwa uangalifu mkubwa shughuli na harakati za makundi yote yenye historia ya vitendo vya kigaidi.

 

Katika duru ya tano ya mazungumzo ya kisiasa baina ya Iran na Ufaransa yaliyosimamiwa kwa pamoja na Sayyid Abbas Araqchi na Gordo Montaigne hapa Tehran, pande mbili zimetilia mkazo wajibu wa kulindwa na kutekelezwa kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA kama ambavyo pia zimejadiliana njia za kuimarisha zaidi uhusiano baina yao.

Katika mazungumzo hayo, Iran na Ufaransa vile vile zimebadilishana mawazokuhusu matukio ya eneo la Mashariki ya Kati na ya kimataifa na kuhimiza kutafutiwa ufumbuzi wa haraka wa kisiasa migogoro hiyo vikiwemo vita vya Yemen.