Jul 08, 2018 12:47 UTC
  • Iran yawakamata magaidi 32 wa ISIS wakiwa wanapanga njama

Mwendesha Mashtaka wa Tehran amesema magaidi wasiopungua 32 wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh wamekamatwa nchini Iran hivi karibuni.

Abbas Jaafari Dowlatabadi Mwendesha Mashtaka wa Tehran amesema: "Wanaume 16 na wanawake 16 kutoka kundi la magaidi wa ISIS ambao walikuwa wamepata mafunzo ya kijeshi nchini Syria, walirejea Iran baada ya kundi hilo kushindwa nchini Syria na walikuwa wanapanga njama ya kutekeleza hujuma za kigaidi kabla ya kukamatwa na maafisa wa usalama." Amesema  faili za magaidi hao sasa ziko mbele ya mahakama.

Jaafari Dowlatabadi ameashiria vitisho vilivyotolewa na kundi la kigaidi la ISIS baada ya wanachame wake wanane kunyongwa hivi karibuni nchini Iran na kusema: "Vitisho hivyo vinaonyesha kuwa Iran imeweza kulishinda kundi la ISIS na haitaruhusu tena ISIS na waungaji mkono wake waendeleze mauaji na ukatili."

Mwendesha Mashtaka wa Tehran ameendelea kubaini kuwa: "Muungaji mkono mkuu wa kundi la kigaidi la ISIS ni serikali ya Marekani ambayo inaliunga mkono kundi hilo ili liibue ghasia na machafuko katika eneo."

Mahakama ikisikilizaj kesi ya magaidi wa ISIS mjini Tehran

Siku ya Jumamosi Shirika la Habari la IRIB lilitangaza habari ya kutekelezwa hukumu ya kunyongwa magaidi wanane wa kundi la ISIS ambao walihusika na hujuma dhidi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, na Haram Takatifu ya Imam Khomeini MA, mjini Tehran Juni 7 mwaka jana.

Katika hujuma hiyo  Wairani 17 waliuawa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa huku magaidi watano nao wakiangamizwa katika makabiliano na vikosi vya usalama vya Iran.

Tags