Waziri Mkuu wa Italia atembelea Iran kuhuisha uhusiano
Rais Hassan Rouhani amesema kuwa Iran inataka kuona uhusiano wa kibiashara na Italia unafika kiwango kilichokuwepo kabla ya nchi hii kuwekewa vikwazo vya nyuklia.
Rais Rouhani amesema hayo hapa mjini Tehran katika mkutano na waandishi habari na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi leo Jumanne.
Ameongeza kuwa, Italia likuwa mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Iran katika Umoja wa Ulaya kabla ya nchi hii kuwekewa vikwazo na hivyo ametaka irejee katika nafasi hiyo.
Umoja wa Ulaya uliiondolea Iran vikwazo kufuatia mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa Julai mwaka jana na kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu. Renzi amewasili Iran mapema leo Jumanne akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa watu 250 na hivyo kumfanya kuwa kiongozi wa ngazi hiyo wa Italia kuitembelea Iran tokea mwaka 2001. Katika safari hiyo ya Renzi mjini Tehran nchi mbili zimetiliana saini mikataba saba ya ushirikiano.
Rais Rouhani alitembelea Italia Januari mwaka huu kwa muda wa siku mbili ambapo nchi mbili zilitia saini mapatano ya kibiashara yenye thamani ya Euro billioni 17.