Mogherini: Majaribio ya makombora ya Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i5167-mogherini_majaribio_ya_makombora_ya_iran_hayakiuki_makubaliano_ya_nyuklia
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa majaribio ya makombora ya Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 16, 2016 16:05 UTC
  • Mogherini: Majaribio ya makombora ya Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa majaribio ya makombora ya Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1.

Bi Federica Mogherini ameyasema hayo leo mjini Tehran katika kikao cha waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake wa Iran, Dakta Muhammad Javad Zarif. Ameongeza kuwa makubaliano hayo ya nyuklia yatafungua njia mbalimbali za ushirikiano wa kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, Iran na umoja huo zimetekeleza ahadi na majukumu yao na kwamba makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na kundi la 5+1 yamekuwa na manufaa kwa nchi zote za Mashariki ya Kati.

Mogherini amewasili mjini Tehran mapema leo akiongoza makamishna 7 wa Umoja wa Ulaya.

Matamshi hayo ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya yanapinga madai yanayotolewa na Marekani kwamba majaribio ya makombora ya balestiki ya Iran yanakiuka makubaliano ya nyuklia.

Mwezi uliopita wa Machi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilifanyia majaribio yaliyofana makombora ya balistiki ya Qader-H, Qader-F na kombora la Qiam.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Dakta Muhammad Javad Zarif amesema katika mkutano huo kwamba majaribio ya makombora ya balestiki ya Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia ya Tehran na 5+1 wala sheria za Umoja wa Mataifa.