Jeshi la Majini la Iran laanza mazoezi ya kijeshi ya Velayat 97
Jeshi la Majini la Iran jana Ijumaa lilianza mazoezi makubwa ya kijeshi yaliyopewa jina la Velayat 97 katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.
Mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika katika eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba milioni mbili kuanzia Lango Bahari la Hormuz, Bahari ya Oman na maeneo ya kusini mwa Bahari ya Hindi.
Mazoezi hayo yanashirikisha zana mbalimbali za kijeshi zikiwemo manuwari za kivita, meli za kurusha makombora, nyambizi kubwa na ndogo, ndege za kivita na helikopta za kikosi cha majini cha kistratijia cha Jeshi la Iran.
Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran, Admiral Hossein Khanzadi amesema kuwa, katika mazoezi ya sasa ya majini jeshi hilo litafanyia majaribio makombora ya Cruise na baharini na makombora ya kulenga manuwari za kivita na nyambizi chini ya maji ya Torpedo na kadhalika.
Mazoezi haya makubwa ya kijeshi ya Velayat 97 yanafanyika miezi kadhaa baada ya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kufanya manuva kubwa ya kijeshi ya aina yake yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu Muhammad (saw) 12 karibu na kisiwa cha Qeshm kilichoko Ghuba ya Uajemi.