Masaibu ya Naibu Rais aliyetimuliwa Kenya, Rigathi Gachagua yazidi, UDA nayo kumtimua
Chama tawala nchini Kenya cha United Democratic Alliance (UDA) kimetangaza kwamba, hivi karibuni kitamteua Naibu Rais mteule, Kithure Kindiki kama naibu kiongozi wa chama hicho mara tu kesi zinazoendelea mahakamani za kupinga kuondolewa madarakani Rigathi Gachagua, zitakapomilika.
Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar jana alisema chama hicho hakitakubali Bw Gachagua kuendelea kuwa naibu kiongozi wa chama kutokana na kudorora uhusiano wake na wabunge na chama hicho kwa kwenda kinyume na maadili yake na kudumaza ajenda yake ya maendeleo ya kitaifa.
“Hili ni suala la kisiasa tu. Hakuna mahakama inayoweza kukupa uongozi. Uhusiano tayari umedorora na huwezi kuendelea kuhudumu kama naibu kiongozi wa chama,” amesema Bw Omar jijini Nairobi.
Amesisitiza kuwa: “Tulikuwa tunasonga mbele kama chama na tulikuwa tumejitolea kuwaunganisha Wakenya bila kujali kabila zao, lakini yeye (Bw Gachagua) anahubiri ukabila na ndiyo maana ilimbidi aondoke."
Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar amesema: “Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya UDA, itatoa tangazo la kujaza nafasi ya Bw Gachagua chamani mara tu mahakama zitakapohitimisha kesi zinazoendelea.
Tarehe 18 Mwezi huu wa Oktoba, Bunge la Kitaifa la Kenya lilidhinisha uamuzi wa Rais wa nchi hiyo, William Ruto, wa kumteua Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa akishikiliwa wadhifa huo, Rigathi Gachagua.
Hata hivyo dakika chache baadaye, Mahakama Kuu nchi hiyo ilitoa amri ya muda ya kusimamisha kubadilishwa kwa Naibu Rais wa nchi hiyo, na kesi kuhusu kadhia hiyo bado inaendelea.
Awali, maseneta wa Kenya walimpata Rigathi Gachagua na hatia ya makosa matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake yakiwemo ya ufisadi, kueneza siasa za chuki na ukabila.