ICC kuthibitisha mashtaka dhidi ya Joseph Kony
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuwa, kikao cha kuthibitisha mashtaka dhidi ya mbabe wa kivita anayesakwa Joseph Kony kitafanyika bila yeye kuwepo mahakamani.
Taarifa ya ICC imesema kuwa, tarehe ya kusikilizwa hoja hizo itatangazwa baadaye. Kony mwenye umri wa miaka 63, amekuwa akisakwa na mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague tangu mwaka 2005.
Anasakwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kufuatia miongo mitatu ya ukatili wa kundi lake la waasi wa Lord's Resistance Army - LRA katika mataifa kadhaa ya Kiafrika.
ICC ilitangaza miezi sita iliyopita kuwa itafanya vikao mwezi huu wa Oktoba kuthibitisha makosa 36 dhidi ya Kony, ambaye hajulikani aliko kwa sasa.
Wakiongozwa na mbabe wa kivita aliyeko mafichoni Joseph Kony, waasi wa LRA waliwatia hofu Waganda kwa takriban miaka 20 wakipigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni kutoka kambi za kaskazini mwa Uganda na nchi jirani. Wanamgambo hao wameangamizwa kwa kiasi kikubwa, lakini Kony anasalia kuwa mmoja wa watoro wanaosakwa sana na mahakama ya ICC.
Genge la Kikristo na la kigaidi la LRA lilianzishwa na Mkatoliki Joseph Kony miongo mitatu iliyopita ambapo Kony alijiita pia nabii.
Ripoti zinaonyesha kuwa, kundi hilo liliwauwa zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 waliolazimishwa kuwa watumwa wa ngono na askari vitani.