Kwa mashinikizo ya Israel, X ilisimamisha akaunti ya Kiongozi Muadhamu na kuifungua baada ya malalamiko ya watumiaji
Parstoday- Baada ya kupita saa 24 za kuisimamisha akaunti ya Ayatullah Ali Khamenei katika mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, imefungua akaunti hiyo ya lugha ya Kiebrania ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Mehdi Fadhaili, mjumbe wa Ofisi ya Kuhifadhi na Kuchapisha Athari za Imamu Khamenei amesema: Akaunti ya Kiebrania ya Kiongozi wa Mapinduzi kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambayo ilianza kwa "Basmillah Rahman Rahim" ilisitishwa katika siku ya pili ya shughuli zake.
Baada ya hatua hii, ambayo iliambatana na malalamiko ya watumiaji wa mtandao wa kijamii wa X, akaunti ya Kiebrania ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika X imefunguliwa.
Mnamo Februari mwaka huu (2024) akaunti za Facebook na Instagram za Ayatullah Khamenei ziliondolewa na Meta, kampuni ya Kimarekani inayoendesha na kumiliki majukwaa hayo mawili.
Akaunti hizo zilifungwa kufuatia mashinikizo ya makundi ya Kizayuni yanayounga mkono Israel ambayo yana ushawishi mkubwa Marekani.
Tangu Oktoba 7, 2023, Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza, Meta imelenga na kuondoa kila maudhui inayoiunga mkono Palestina kwenye majukwaa yake ya Instagram na Facebook.
Katika upande wa pili X, Instagram na Facebook zimejiepusha kuchukua hatua dhidi ya akaunti zozote zinazomilikiwa na maafisa wa Israel ambao wamekuwa wakichochea mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Hesabu za kurasa za mitandao ya kijamii za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu zinazuiwa na kufungwa katika mitandao ya kijamii katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni shakhsia, maafisa na hata watumiaji wenye historia mbaya katika nchi za Magharibi wamekuwa wakitumia kila kisingizio kuunga mkono uenezaji wa chuki dhidi ya Uislamu, kuvunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu (Qur'ani) na Mtume Muhammad (SAWW) kwenye kurasa za mitandao ya kijamii.