Maelfu wahamishwa baada ya Al-Shabab kudhibiti mji katikati mwa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128368
Afisa mmoja wa jeshi la Somalia ametangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabab wameuteka mji wa Tardo katika eneo la Hiiran katikati ya nchi hiyo.
(last modified 2025-07-16T02:53:00+00:00 )
Jul 15, 2025 16:22 UTC
  • Maelfu wahamishwa baada ya Al-Shabab kudhibiti mji katikati mwa Somalia

Afisa mmoja wa jeshi la Somalia ametangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabab wameuteka mji wa Tardo katika eneo la Hiiran katikati ya nchi hiyo.

Meja Mohamed Abdullahi amevieleza vyombo vya habari kuwa, mji wa Tardo, ambao ni njia kuu kati ya vituo vikubwa vya mijini ulitoka kwenye udhibiti wa vikosi vya serikali baada ya wapiganaji wa Al-Shabab kuwatimua wapiganaji wa koo zinazoshirikiana na serikali ya Mogadishu.

Mbunge wa Somalia Dahir Amin amesema, familia zipatazo 12,500 zimeikimbia Tardo na mji wa karibu wa Muqokori, ambao Al-Shabab waliuteka wiki iliyopita.

Kundi hilo la kigaidi linaendelea kusonga mbele ili kuyadhibiti maeneo mengine katika eneo hilo. Takribani askari 100 wa jeshi la Somalia wametumwa ili kutoa msukumo wa mashambulizi ya kujibu mapigo yanayoongozwa na wapiganaji wa koo.

Al-Shabab ambao wana uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, walianzisha uasi nchini Somalia 2007, katika jaribio la kuipindua serikali ya nchi hiyo.

Mashambulizi ya Al-Shabab katika eneo la Hiiran yalipamba moto tangu mapema mwaka huu.

Upigaji hatua wa awali wa Al-Shabab ulifika hadi kilomita 50 kutoka mji mkuu Mogadishu, lakini vikosi vya Somalia vilifanikiwa kuvikomboa baadhi ya vijiji vya mji huo.../