Waandishi 1000 mashuhuri duniani kususia taasisi za kitamaduni za Israel
Zaidi ya waandishi elfu moja wameahidi kutoshirikiana na taasisi za kiutamaduni za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambazo zinatajwa kushiriki katika ukiukaji wa haki za Wapalestina.
Katika taarifa yao ya pamoja, waandishi hao wameeleza kuwa, ushirikiano na taasisi za kiutamaduni za utawala wa Kizayuni wa Israel unaweza kusaidia kutekelezwa sera na mienendo ya kibaguzi, jambo ambalo litahalalisha uvamizi, ubaguzi wa rangi na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sally Rooney, Rachel Kushner, na Arundhati Roy ni miongoni mwa waandishi 1,000 mashuhuri ambao wameahidi katika taarifa ya pamoja kutoshirikiana na wachapishaji, tamasha au machapisho ya taasisi za kiutamaduni za Israel ambazo "zinashiriki katika kukiukwa haki za Wapalestina."
Rooney, mwandishi wa kitabu "Watu wa Kawaida" (Ordinary People) na hivi karibuni "Intermezzo," amekuwa mtetezi wa haki za Wapalestina kwa muda mrefu, na mwaka 2021 alikataa kuuza haki za tarjumi ya Kiebrania ya riwaya yake ya tatu, "Beautiful World, Where Are You" kwa mchapishaji wa Kizayuni.
Baada ya kupokea Tuzo ya PEN Pinter mapema mwaka huu, Rooney alitumia nafasi hiyo kutoa hotuba akizungumzia masaibu ya watu wa Gaza, akisema atatoa tuzo yake kwa Mfuko wa Watoto wa Palestina.
Taarifa iliyotolewa na zaidi ya waandishi elfu moja inaendelea kusema: Taasisi ambazo hazijawahi kuzitambua hadharani haki zisizoweza kubatilishwa za watu wa Palestina, ambazo zimeainishwa katika sheria za kimataifa, zitawekewa vikwazo.
Waandishi hao wamesema: Huko nyuma waandishi wengi waliopinga sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, apartheid, walichukua msimamo kama huu kwa sababu dhamiri ya binadamu haituruhusu tuwe na tabia ya kutojali ubaguzi wa rangi na ukimbizi wa kisasa wala kushirikiana na taasisi za utawala wa Kizayuni.