Pentagon: Marekani imejitolea kuiunga mkono Israel dhidi ya Iran
(last modified Wed, 30 Oct 2024 12:40:59 GMT )
Oct 30, 2024 12:40 UTC
  •  Pentagon: Marekani imejitolea kuiunga mkono Israel dhidi ya Iran

Jenerali Patrick Ryder, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon amesema kuwa, Washington inafuatilia hali iliyopo huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa na hofu ya kuandamwa na jibu la kijeshi la Iran kutokana na hujuma yake ya hivi karibuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ryder amewaambia waandishi wa habari: "tunafuatilia hali ya mambo na tumejitolea kusaidia Israel dhidi ya Iran."

"Lazima tujiweke tayari kwa kila liwezekanalo. Ikiwa Iran itachukua hatua yoyote dhidi ya Israel, tumejitolea kuilinda Israel"  ameeleza msemaji huyo wa Pentagon wakati akijibu maoja ya maswali aliyoulizwa.

Ryder amezungumzia pia mazungumzo ya hivi majuzi kati ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri wa Vita wa Israel Yoav Gallant kuhusu usitishaji vita huko Ukanda wa  Gaza.

Hali ni ya wasiwasi mkubwa katika eneo la Asia Magharibi tangu utawala bandia wa  Israel ulipofanya mashambulizi dhidi ya Iran ikidai ni ya kujilinda, mashambulio ambayo yamelaaniwa kimataifa.

Sayyid Abbas Araghchi

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza la Usalama na wa Baraza Kuu kufuatia hujuma ya Israel dhidi ya Iran.

Katika barua yake, Araghchi ameieleza bayana Jamii ya Kimataifa kuwa uchokozi huo uliofanywa na Israel hautapita bila kujibiwa, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran inabaki nayo haki yake ya msingi ya kujibu mashambulizi dhidi ya mamlaka yake ya kitaifa ya kujitawala kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.