Malalamiko ya wajumbe wa Baraza la Usalama dhidi ya ushirikiano wa Marekani na utawala wa Kizayuni
Katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika karibuni kwa ajili ya kijadili suala la hujuma ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi nyingi zikiwemo Algeria, China, Russia, Iraq na Syria zimelaani vikali kitendo hicho cha uchokozi na kutaka uchokozi huo ukomeshwe mara moja.
Kikao hicho kimefanyika kwa ombi la Iran na baada ya utawala wa Kizayuni kushambulia baadhi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam Jumamosi asubuhi ya tarehe 26 Oktoba, ambapo askari wanne wa Iran waliuawa shahidi. Pamoja na hayo mfumo jumuishi wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliweza kukabiliana kwa mafanikio na hatua hiyo ya kichokozi ya utawala huo bandia.
Amir Saeid Iravani, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao hicho kwamba uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Iran ni wa wazi na wa mara kwa mara. Mashambulizi hayo ya kichokozi ni sehemu ya mwelekeo mpana na endelevu wa uchokozi na kutowajibishwa utawala wa Israel, ambapo unaendelea kulivuruga eneo hili hususan kupitia uvamizi usiokoma, mauaji ya kikabila na jinai za vita dhidi ya wananchi wa Palestina na Lebanon.
Katika kikao hicho nchi za eneo sambamba na kulaani jinai za kinyama za utawala pandikizi wa Israel zimetoa wito wa kulaaniwa kimataifa hatua hizo za utawala wa Kizayuni na kutoungwa mkono na nchi za Magharibi, hususan katika kushadidisha vita katika eneo. Vasily Nebenzya, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, ameonya vikali juu ya "msururu usiodhibitiwa" wa ghasia Asia Magharibi kufuatia mashambulio ya Israeli dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema, eneo sasa limevurugika kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na kuongezeka ghasia katika Ukanda wa Gaza.
Ammar bin Jame, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Algeria katika Umoja wa Mataifa pia amesema: "Mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Iran ni ukiukaji wa amani ya kimataifa."
Kutokana na kuwa uvamizi na uchokozi wa utawala habithi wa Israel unafanyika kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani, katika kikao cha Baraza la Usalama pia, nchi za Magharibi zimeendelea kuunga mkono utawala huo bila masharti na kupuuza jinai zake na wakati huo huo kujaribu kuonyesha kuwa Iran ndiyo imesababisha hali ya hivi sasa katika eneo. Kuhusiana na hilo Linda Thomas Greenfield, mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amedai kuwa Marekani haikushiriki katika mashambulio ya karibuni yaliyotekelezwa na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuitaka Iran isitishe mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala huo.
Nchi za Magharibi zinaitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutojibu uchokozi wa utawala wa Kizayuni, katika hali ambayo Iran daima imekuwa ikizipa kipaumbele siasa za kuimarisha ushirikiano na nchi jirani na za eneo na kuzuia uingiliaji wa nchi za kigeni. Kwa mantiki hiyo, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Amir Saeid Iravani amesisitiza kuwa: Iran daima imekuwa ikichukulia diplomasia kama njia ya kutatua changamoto za eneo na kuimarisha amani na utulivu.
Kuhusiana na hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazichukulia hatua za makusudi na za kichokozi za utawala wa Kizayuni kuwa ni kukiuka wa misingi ya sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa, hasa ibara ya 2, kipengele cha 4 ambacho kinaeleza wazi kwamba matumizi ya nguvu dhidi ya mamlaka na ardhi ya nchi yoyote ile ni kinyume cha sheria. Hivyo kukabiliana na ukiukaji na uchokozi huo wa Israel ni haki halali na ya kisheria ya Iran.
Vile vile inapaswa kuzingatiwa kuwa matukio ya miongo ya hivi karibuni hasa katika eneo la Asia Magharibi yanathibitisha wazi kuwa, sababu kuu ya ukosefu wa usalama katika eneo, kuenea ugaidi, ukosefu wa amani na kushadidi migogoro katika nchi za eneo ni utawala wa Kizayuni na uingiliaji wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi. Kuhusiana na hilo, uungaji mkono usio na kikomo wala masharti wa Marekani na waitifaki wake kwa utawala ghasibu wa Israel umepelekea hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lina jukumu la kusimamia amani na usalama katika maeneo tofauti ya dunia kushindwa kutekeleza wajibu wake.