Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Trump si mtu wa kubadilishana naye jumbe
Akiwa katika siku ya pili ya safari yake hapa nchini, Abe Shinzo (Shinzo Abe) Waziri Mkuu wa Japan siku ya Jumatano asubuhi alikutana na kuzungumza na Ayatullah Khameneii, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Japan alimwambia Kiongozi Muadhamu: Ninataka kukufikikishia ujumbe wa rais wa Marekani. Kiongozi Muadhamu alimjibu kwa kusema: Hatuna shaka yoyote kuhusiana na nia yako njema lakini kuhusu yale uliyonukuu kutoka kwa rais wa Marekani, kwa kweli mimi simuoni Trump akiwa mtu anayefaa kubadilishana naye ujumbe wowote na sina jibu lolote kwake, wala sitamjibu.'
Kiongozi Muadhamu alisema: Mambo nitakayoyazungumza katika kikao hiki yatahusiana tu na Waziri Mkuu wa Japan kwa sababu tunaichukulia Japan kuwa nchi rafiki, hata kama tuna baadhi ya malalamiko kuihusu.
Kuhusu matamshi ya Waziri Mkuu wa Japan kwamba Marekani iko tayari kufanya mazungumzo ya kweli na Iran, Kiongozi Muadhamu alisema: Kwa muda wa miaka mitano sita hivi, Jamhuri ya Kislamu ya Iran ilifanya mazungumzo na Marekani pamoja na nchi za Ulaya katika fremu ya kundi la 5+1 na kufikia matokeo fulani, lakini baada ya hapo Marekani iliyakiuka. Hivyo ni mtu gani aliye na akili timamu anaweza tena kufanya mazungumzo na nchi kama hii isiyoheshimu mapatano?
Kuna mifano mingi sana inayoweza kutolewa ushahidi hapa. Kwa mfano Ayatullah Khamenei aliashiria mazungumzo ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani na Waziri Mkuu wa Japan kuhusiana na Iran na kusema: Trump mara tu baada ya kumalizika mazungumzo hayo alirejea nchini kwake na kuiwekea vikwazo sekta ya petrokemikali ya Iran. Je, ujumbe huo ni wa nia njema? Je, jambo hilo linaonyesha kwamba kweli rais huyo anataka mazungumzo yenye nia njema?
Kiongozi Muadhamu aliashiria matamshi ya Waziri Mkuu wa Japan kwamba Marekani inataka Iran isimiliki silaha za nyuklia na kusisitiza tena msimamo wa Iran kuhusu silaha hizo kwa kusema: Sisi tunapinga silaha za nyuklia na tayari tumeshatoa fatwa inayoharamisha utengenezaji wa silaha hizo. Pamoja na hayo, elewa vyema suala hili kwamba hata kama tungetaka kutengeneza silaha za nyuklia, Marekani haingefanya lolote na kutotoa idhini kwake hakungezuia chochote. Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba urundikaji wa silaha za nyuklia pia kunakinzana na akili salama na kusema: Marekani haina ustahiki wowote wa kusema ni nchi gani inapasa kuwa na silaha za nyuklia na ni ipi isiyofaa kuwa na silaha hizo kwa sababu nchi hiyo yenyewe ina maelfu ya vichwa vya silaha hizo katika maghala yake ya silaha.
Ukweli ni kwamba Marekani haiichukii Iran kutokana na shughuli zake za nyuklia wala mapatano ya JCPOA, bali kufikia sasa, Trump kama anavyodai mwenyewe, ametumia kila njia na hatua inayoweza kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuzuia maendeleo yake. Ni kwa kuzingatia uzoefu na ukweli huo ndipo Kiongozi Muadhamu akajibu matamshi ya Waziri Mkuu wa Japan akimnukuu Trump kwamba, hana nia ya kuupindua mfumo wa Kislamu wa Iran kwa Kusema: Tatizo letu na Marekani sio suala la kuupindua mfumo kwa sababu hata kama wana nia kama hiyo hawawezi kuitekeleza kivitendo. Kama ambavyo katika kipndi cha miaka 40 iliyopita, marais wa Marekani waliomtangulia Tump walifanya juhudi kubwa za kuiangamiza Iran lakini wakashindwa kufikia lengo hilo.
Noam Chomsky, mwananadharia na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Marekani anatoa tathmini yake kuhusiana na sababu hasa za Marekani kuichukia Iran kwa kusema: Moja ya masuala muhimu katika uhusiano wa kimataifa yasiyojadiliwa katika vitabu vya nadharia ni kuhusiana na suala la umafia. Masuala ya kimataifa huendeshwa kimafia. Marekani huwa haivumilii kuona amri zake zikipuuzwa.
Huu ni ukweli ambao hata Abe Shinzo mwenyewe aliukubali katika mazungumzo yake na Kiongozi Muadhamu aliposema Wamarekani daima hutaka kuzilazimisha nchi nyingine zifuate fikra na itikadi zao.
Kwa msingi huo si jambo gumu kudiriki na kufahamu ni kwa nini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina imani na Marekani na kutokuwa na faida yoyote kufanya mazungumzo na nchi kama hiyo. Pamoja na hayo jambo lililokuwa na umuhimu katika mazungumzo hayo ni Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kukaribisha pendekezo la Waziri Mkuu wa Japan la kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi. Alisema: Japan ni nchi muhimu barani Asia na iwapo ina nia ya kuimarisha uhusiano wake na Iran inapasa kuthibitisha kivitendo nia hiyo, kama zilivyofanya nchi nyingine muhimu kuhusu jambo hilo.