Waziri Mkuu Malaysia: Marekani isijaribu kuivamia kijeshi Iran
Waziri Mkuu wa Malaysia amewaonya viongozi wa Marekani kuwa wasijaribu kuingia vitani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mahathir Bin Mohamad ameyasema hayo leo kando na mkutano wa viongozi wa Umoja wa Nchi za Kusini mwa Bara la Asia (ASEAN) mjini Bangkok, mji mkuu wa Thailand na kuongeza kuwa, kukosea mahesabu kwa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kunaweza kuibua vita vya dunia. Amebainisha kwamba iwapo Wamarekani wataingia vitani dhidi ya Iran, basi watatakiwa kufahamu kwamba sio Iran pekee itakayoikabili Marekani, bali hata nchi nyingine ambazo hazipo tayari kuona silaha za nyuklia zikitumiwa, nazo zitalazimika kuingia katika vita hivyo kwa lengo la kuzuia silaha hizo.
Onyo la Waziri Mkuu wa Malaysia kwa Marekani limetolewa katika hali ambayo, viongozi wa Washingto wamekuwa wakipiga ngoma ya vita dhidi ya Iran ya Kiislamu. Katika uwanja huo hivi karibuni Rais Donald Trump alidaiwa kutoa amri kwa jeshi la nchi yake kwa ajili ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran, amri ambayo hata hivyo aliibatilisha haraka sana baadaye. Amri hiyo ilitolewa baada ya ndege ya kijasusi ya Marekani isiyo na rubani aina ya RQ-4 Global Hawk na ambayo ndio ya kisasa kabisa kwa jeshi la Marekani, kuangamizwa na jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) baada ya ndege hiyo kuingia katika anga ya maji ya Iran.