Amir Hatami: Wanaodai kutetea haki za binadamu hawaoni jinai zinazofanyika Yemen?
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa mauaji yanayoendelea kufanywa katika eneo la Mashariki ya Kati dhidi ya watu wasio na hatia hususan watu wanaodhulumiwa wa Yemen kwa kutumia silaha za nchi za Magharibi ni ukurasa mwingine wa jinai za nchi za Magharibi unaosajiliwa katika historia.
Brigedia Jenerali Amir Hatami ameashiria jinsi baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani zilivyoupa utawala wa Baath nchini Iraq silaha za kemikali na kusema: Nchi hizo zinazodai kutetea haki za binadamu zinapaswa kuwajibika mbele ya walimwengu kutokana na jinai zilizofanyika miaka ya nyuma na zinazoendelea kufanyika.
Waziri wa Ulinzi wa Iran ambaye alikuwa akizuungumza kwa mnasaba wa siku ya leo tarehe 28 Juni ambayo imetangazwa hapa nchini kuwa ni Siku ya Kitaifa ya Kukabiliana na Silaha za Kemikali na za Sumu amesema kuwa, siku hiyo inakumbusha ukurasa mwingine wa jinai za dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein ambaye alitumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji na wananchi wa miji na vijiji vya Iran katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu.
Brigedia Jenerali Hatami ameashiria jitihada zinazofanywa na nchi za Magharibi za kutaka kufuta na kukana mchango wao wa kumuwezesha Saddam Hussein kupata silaha za kemikali na kusema: Nchi za Magharibi zinakiri kwamba Wairani elfu 20 waliuawa shahidi katika mashambulizi ya silaha za kemikali za Sadddam Hussein. Amesema jinai kubwa zaidi ya silaha za kemikali za Saddam ilifanyika katika eneo la Sardasht tarehe 28 Juni mwaka 1987 ambapo raia 119 wa eneo hilo waliuawa shahidi na maelfu ya wengine walijeruhiwa.