Dakta Javad Zarif: Iran haitafanya mazungumzo na magaidi
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, sera za Marekani za kuliwekea vikwazo taifa la Iran ni ugaidi na kwamba, Iran haitafanya mazungumzo na magaidi.
Dakta Zarif amesema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini New York na kubainisha kwamba, Marekani imeshughulishwa na vita vya kiuchumi dhidi ya Iran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, vita vya kiuchumi ambavyo vinatajwa kwa ufakhari na Rais Donald Trump vimewalenga raia.
Dakta Zarif ameongeza kuwa, hatua hiyo ya Marekani ni ya kigaidi; kwani ugaidi ndio ambao huwalenda wananchi ili kusukuma mbele mipango yake ya kisiasa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema bayana kwamba, maana ya ugaidi ni kufanya juhudi kwa kutumia ubabe ili kubadilisha siasa za nchi fulani au kuwalazimisha wananchi wabadilishe siasa zao.
Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitumia mashinikizo makali zaidi na vitisho ili kwa dhana yake ailazimishe Iran ikubali kukaa katika meza ya mazungumzo na Washington.
Hata hivyo Iran imesimama kidete na kwa nguvu zake zote na hivyo kufanikiwa kusambaratisha njama za zote za Washington dhidi yake.
Hivi karibuni Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, katika kipindi cha miezi 14 iliyopita, Marekani imetekeleza vikwazo vikali kabisa dhidi ya taifa la Iran, hata hivyo imeshindwa katika nyanja zote iwe ni katika uga wa kijamii, kisiasa na kadhalika.