Marekani yaendeleza uraibu wa vikwazo, yamuwekea vikwazo Zarif
Wizara ya Fedha ya Marekani imeendeleza uraibu wa nchi hiyo wa kuziwekea vikwazo nchi mbalimbali kwa kuliweka jina la Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na nchi hiyo.
Wizara ya Fedha ya Marekani mapema leo Alkhamisi kwa wakati wa Tehran imeliweka jina la Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na seikali ya Washington.
Itakumbukwa kuwa tarehe 4 Julai mwaka huu Dakta Zarif alisema katika mahojiano yake na gazeti la New York Times kuhusu uwezekano wa kuwekewa vikwazo na Marekani kwamba, hana tatizo lolote na vikwazo hivyo. Muhammad Javad Zarif aliongeza kuwa, yeye na watu wa familia yake hawana milki wala akaunti za fedha katika benki za nje ya Iran na kusema: Iran ndiyo maisha na kila kitu chake.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alisema kuwa taathira pekee ya hatua ya Marekani ya kuliweka jina lake katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo ni kubana na kupunguza uwezo wake wa kutengeneza mahusiano.
Oktoba mwaka jana pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alijibu hatua ya Marekani ya kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran kwa kusema: Uraibu wa kuweka vikwazo wa Marekani sasa haudhibitiki.