Zarif: Uvamizi wa Israel umethibitisha kwamba, kuanzisha uhusiano na Israel hakuna faida
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza haki ya Wapalestina ya kujitetea mbele ya dhulma na ukandamizaji wa utawala wa kiapathaidi wa Israel na kusema kuwa, kuporwa na kughusubiwa kitongoji kingine cha Waarabu pambizoni mwa Msikiti wa al-Aqswa kumethibitisha kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida baadhi ya nchi za Kiarabu na Israel hakuna faida yoyote.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika taarifa yake iliyosomwa na Majid Takht-Ravanchi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili kadhia ya Palestina pamoja na matukio ya taifa hilo madhulumu.
Dakta Zarif amesema katika ujumbe wake huo kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendesha siasa za kibaguzi na ubaguzi wa rangi aina ya apathaidi chini ya anuani ya 'nchi ya Kiyahudi' umekuwa ukipinga kwa nguvu zote haki ya Wapalestina ya kujiainishia hatima na mustakabali wao.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuashiria mauaji na uharibifu mkubwa uliofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza amekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa na asasai mbalimbali za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Sehemu nyingine ya ujumbe huo inasema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena inasisitiza uungaji mkono na mfungamano wake kwa malengo matukufu ya Palestina na itaendelea kuheshimu ahadi yake ya kuliunga mkono taifa la Palestina ambalo linafanya juhudi ya kupigania haki zake halali.