Umoja wa Afrika: Mateso dhidi ya Wapalestina lazima yakomeshwe
Mahmoud Ali Youssouf Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amesema kuwa, mauaji dhidi ya wananchi wa Palestina ni lazima yakomeshwe. Mahmoud Ali Youssouf alisema hayo jana (Jumamosi) wakati akiufungua mkutano wa kilele wa 39 wa umoja huo.
Akihutubia katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia, Mahmoud Ali Youssouf alisema vita na mateso kwa watu wa Ukanda wa Gaza yanatoa changamoto kubwa katika dhamira ya bara hilo.
Eneo hilo dogo la Gaza limekuwa chini ya mzingiro mkali wa utawala ghasibu wa Israel tangu kuanza vita vya mauaji ya kimbari ya Israel Oktoba 7 mwaka 2023.
Tangu wakati huo utawala haramu wa Israel umekuwa ukiushambulia Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 71, 000.
Ripoti mbalimbali za mashirika ya kieneo na kimataifa zimeonya kuhusiana na ukatili unaofanywa na Israel kwa uungaji mkono wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.
Aidha Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), aligusia migogoro mengine inayoendelea barani Afrika ikiwemo Sudan, akisema kuwa, watu wa bara hilo wanaendelea kuishi katika mazingira yasio na usalama.
"Kuanzia Sudan hadi Sahel, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Somalia na kwingineko, watu wetu wanaendelea kulipa gharama kubwa ya ukosefu wa utulivu", amebainisha afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika
Mkutano wa kilele wa 39 wa Umoja wa Afrika ulifunguliwa jana J asubuhi, Februari 14, huko Addis Ababa, Ethiopia. Wakuu wa nchi na serikali zaidi ya hamsini wanashiriki katika mkutano huo na kauli mbinu ya mwaka huu ni maji safi.