Sayyid Abbas Mousavi: Iran inakaribisha kwa mikono miwili ushirikiano na majirani zake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55253-sayyid_abbas_mousavi_iran_inakaribisha_kwa_mikono_miwili_ushirikiano_na_majirani_zake
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni suala la kuimarisha ushirikiano na majirani zake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2019 03:37 UTC
  • Sayyid Abbas Mousavi: Iran inakaribisha kwa mikono miwili ushirikiano na majirani zake

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni suala la kuimarisha ushirikiano na majirani zake.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo leo na kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kwa mikono miwili ushirikiano na majirani zake ambao huko nyuma walikuwa na suitafahamu na Iran lakini sasa wanaonekana kubadilisha misimamo na utendaji wao.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kubadilisha msimamo na utendaji baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi kuhusiana na Iran na kueleza kwamba, endapo itafikia siku nchi za eneo zifikie natija hii kwamba, zina haja ya kushirikiana na Iran kwa ajili ya usalama wao, wa eneo na wa kimataifa, basi Tehran inakaribisha kwa moyo mkunjufu kabisa uamuzi huo.

Brigedia Jenerali Qasem Rezai Kamanda wa kikosi cha walinzi wa mpakani cha jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (kulia) na Brigedia Jenerali Muhammad Ali Misbah al-Ahbabi kamanda wa gadi ya pwani ya Imarati walipokutana hivi karibuni mjini Tehran

Kufanyika hivi karibuni kikao cha pamoja cha kamanda wa kikosi cha walinzi wa mpakani cha jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kamanda wa gadi ya pwani ya Imarati katika fremu ya kuimarishwa uhusiano wa kidiplomasia wa nchi mbili na kudhaminiwa usalama wa Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ni ishara ya wazi inaoonyesha kuweko azma na irada thabiti ya kisiasa ya kuleta  anga ya ushirikiano baina ya pande mbili hizo..