Zarif ahimiza kusainiwe mapatano ya kutoshambuliana, Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55457-zarif_ahimiza_kusainiwe_mapatano_ya_kutoshambuliana_ghuba_ya_uajemi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza tena udharura wa kuwepo mazungumzo baina ya nchi za kanda ya Ghuba ya Uajemi kuhusu mkataba wa kutoshambuliana.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 18, 2019 12:41 UTC
  • Zarif ahimiza kusainiwe mapatano ya kutoshambuliana, Ghuba ya Uajemi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza tena udharura wa kuwepo mazungumzo baina ya nchi za kanda ya Ghuba ya Uajemi kuhusu mkataba wa kutoshambuliana.

Dakta Muhammad Javad Zarif ambaye yuko safarini nchini Kuwait ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba, katika mazungumzo yake na Mrithi wa Amir wa Kuwait na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo pande mbili zimebadilishana mawazo kuhusiana na pendekezo la Iran la kufanya mazungumzo baina ya nchi za kanda hii kuhusu mkataba wa kutoshambuliana. 

Zarif ameongeza kuwa: Pendekezo la Iran la kuwepo mazungumzo baina ya nchi za kanda ya Ghuba ya Uajemi ni bora sana kuliko kuwa tegemezi kwa majeshi ya nchi ajinabi.  

Katika mazungumzo yake ya leo na Mrithi wa Amir wa Kuwait, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametilia mkako udharura wa kudumishwa ushirikiano wa kikanda na kusema nchi za eneo hilo zitaendelea kuwepo hapo na maajinabi wataondoka. 

Zarif akizungumza na Mrithi wa Amir wa Kuwait

Ameutaja uhusiano wa Iran na Kuwait kuwa ni wa kidugu na kirafiki na akahimiza suala la kuimarishwa zaidi uhusiano huo. Vilevile amemtakia afya na ahueni Amir wa Kuwait Sabah al Ahmad Jabir al Sabah na kumtaja kuwa ni miongoni mwa viongozi wenye uelewa mkubwa katika eneo la Ghuba ya Uajemi. 

Zarif aliwasili Kuwait jana usiku kwa shabaha ya kukutana na kubadilishana mawazo na viongozi wa nchi hiyo.