Zarif: Wakala wa IAEA ufanye kazi kitaalamu bila ya upendeleo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unapaswa kutekeleza majukumu yake kitaalamu, kwa usiri na bila ya kupendelea upande wowote.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika maungumzo yake na Cornel Feruta, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) aliyeko safarini mjini Tehran na kuongeza kuwa: hatua ya Iran na kupunguza utekelezaji wa majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA imechukuliwa mkabala wa hatua ya nchi za Ulaya ya kutotekeleza majukumu yao ndani ya makubaliano hayo, na yote hayo yanafanyika kwa mujibu wa kifungu nambari 36 cha makubaliano ya JCPOA.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria ushirikiano mkubwa wa Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki uliopelekea kutolewa ripoti kadhaa zilizothibitisha kuwa, Iran imetekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Cornel Feruta ameashiria jitihada zinazofanywa na wakala huo kwa ajili ya kujenga hali ya kuaminiana na kutilia mkazo udharura wa kufanyika shughuli za wakala huo kitaalamu na bila ya kupendelea upande wowote.
Cornel Feruta aliwasili jana mjini Tehran kwa shabaha ya kufanya mazungumzo na maafisa wa ngai za juu wa Iran.
Jana Jumapili alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) Ali Akbar Salehi ambapo pande hizo mbili zilibadilishana mawazo kuhusiana na masuala mbalimbali.
Feruta aliyemrithi Yukia Amano ambaye aliaga dunia mwezi Julai mwaka huu akiwa na umri wa miaka 72, amekutana pia na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Iran.