Zarif awataka wavamizii 'walioshindwa' nchini Afghanistan waondoke
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuhusiana madola ya kigeni kuitumia vibaya hali ya sasa nchini Afghanistan na kuvitaka vikosi vya kigeni ambavyo vimeshindwa kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo.
Dakta Muhammad Javad Zarif ameonyesha wasiwasi alionao kuhusiana na hali inayotawala hivi sasa nchini Afghanistan na kusema kuwa, kwa mtazamo wa Iran wavamizi wanapaswa kukubali kwamba, wameshindwa na hivyo kuondoka mara moja kutoka katika nchi hiyo.
Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka pande zinazozozana nchini Afghanistan kupiga moyo konde na kuacha kuuana wao kwa wao.
Dakta Zarif amezitaka pia pande hizo kusitisha mauaji hadi pale kutakapopatikana usitishaji vita wa kudumu.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran inaheshimu mamlaka ya kujitawala Afghanistan na inaona kuna udharura wa wananchi wa nchi hiyo kusimamiia na kuongoza mchakato wowote ule wa amani.
Katika miezi ya hivi karibuni ukosefu wa amani umeongezeka nchini Afghanistan kupitia hujuma, mashambulio na milipuko ya kigaidi.
Ukosefu wa amani unaongezeka nchini Afghanistan katika hali ambayo, Marekani na waitifaki wake wametuma majeshi nchini humo tangu mwaka 2001 kwa kisingiizio cha kupambana na ugaidi na kudhamini amani na usalama wa nchi hiyo.
Viiongozi wa Kabul wanasisitiza kuwa, uwepo wa vikosi vya kigeni nchini Afghanistan haujasaidia chochote ghairi ya kuongeza machafuko, ugaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya.