Zarif: Mashambulizi dhidi ya Iran yatasababisha vita kubwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56124-zarif_mashambulizi_dhidi_ya_iran_yatasababisha_vita_kubwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa Iran iko tayari kujihami wakati wowote ule na kwamba, shambulizi lolote dhidi ya Iran litasababisha vita vya pande zote na kupelekea kuuawa idadi kubwa ya wavamizi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 19, 2019 22:30 UTC
  • Zarif: Mashambulizi dhidi ya Iran yatasababisha vita kubwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa Iran iko tayari kujihami wakati wowote ule na kwamba, shambulizi lolote dhidi ya Iran litasababisha vita vya pande zote na kupelekea kuuawa idadi kubwa ya wavamizi.

Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akizungumza na televisheni ya CNN ya Marekani amezitahadharisha Washington na Riyadh kuhusu shambulizi la aina yoyote dhidi ya Iran na kusema: Jamhuri ya Kiislamu haijawahi kutaka vita na haitaki kuona eneo la Ghuba ya Uajemi likitumbukia vitani. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria tuhuma za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na operesheni ya kulipiza kisasi ya wapiganaji wa Yemen dhidi ya taasisi za mafuta za Saudi Arabia na kusema: Tehran haikuhusika na mashambulizi hayo, na jeshi la Yemen limetangaza waziwazi kuwa ndilo lililotekeleza operesheni hiyo.

Amesisitiza kuwa watu wa Yemen wanajihami mkabala jinai zinazoendelea kufanywa na Wasaudia na mauaji ya halaiki dhidi ya watoto na familia zao.

Watoto wa Yemen wanaendelea kuuawa katika mashambulizi ya Saudiia.

Zarif pia amesema kuwa hakuna uwezekano wa kufanyika mazungumzo baina ya Iran na Marekani na kuongeza kuwa, Tehran haiwezi kufanya mazungumzo na serikali ya Donald Trump kabla ya Marekani haijaondoa vikwazo vyote kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA. 

Jumamosi iliyopita, kikosi cha drone cha harakati ya Ansarullah kilishambulia viwanda vya kusafisha mafuta vya Buqayq na Khurais vya shirika la mafuta la Saudia, ARAMCO na kusababisha hasara kubwa kwa Riyadh. Mashambulizi hayo ambayo yamesimamisha nusu ya uzalisha wa mafuta yote ya Saudi Arabia, yamefanyika kujibu jinai na mauaji yanayoendelea kufanywa na watawala wa Riyadh dhidi ya raia wa Yemen.