Zangeneh: Inawezekana kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi bila madola ajinabi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56408-zangeneh_inawezekana_kudhamini_usalama_wa_ghuba_ya_uajemi_bila_madola_ajinabi
Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kushirikiana na nchi nyingine za eneo kwa ajili ya kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari na Hormuz.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2019 03:49 UTC
  • Zangeneh: Inawezekana kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi bila  madola ajinabi

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kushirikiana na nchi nyingine za eneo kwa ajili ya kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari na Hormuz.

Bijan Zangeneh amesema hayo mwishoni mwa safari yake ya siku mbili huko Moscow Russia alilokwenda kushiriki katika mkutano wa Jukwaa la Nchi Zinazosafirisha Gesi na kusisitiza kwamba, ili kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz hakuna haja kabisa ya kutegemea uwepo wa madola ya kigeni katika maeneo hayo.

Waziri wa Mafuta wa Iran amesema kuwa, daima Tehran imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa, matatizo yaliyopo katika eneo hili yanapatiwa ufumbuzi.

Bijan Zangeneh ameongeza kuwa, nchi za eneo zinaitambua Iran kama rafiki yao.

Bijan Zangeneh, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Kadhalika Waziri wa Mafuta wa Iran ameashiria misimamo na hatua za upande mmoja za Marekanii na kusema kuwa, maamuzi ya upande mmoja yanabadilika na kuwa tishio kwa dunia na kwamba, hata madola ya Ulaya hayakubaliani na msimamo huo wa Washington.

Zangeneh ameashiria mkutano wa Jukwaa la Nchi Zinazosafirisha Gesi na kusema kuwa, Russia inapinga madai ya Saudia ya kuituhumu Iran kwamba, ilihusika katika mashambulio dhidi ya taasisi ya mafuta ya ARAMCO kwani hakuna nyaraka na ushahidi wowote ule wa kuthibitisha madai hayo ya utawala wa Aal Saud na washirika wake.