Ethiopia yailaumu Misri kwa kukwamisha mazungumzo kuhusu bwawa la al Nahdha
Serikali ya Ethiopia imeilaumu Misri kwa kukwamisha mazungumzo kuhusiana na bwawa la al Nahdha linalojengwa na Ethiopia kwa ajili ya kufaidika na maji ya Mto Nile.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema kupitia televisheni ya taifa kwamba upande wa Misri ndio unaopaswa kulaumiwa kwa kufeli mazungumzo hayo.
Televisheni ya Ethiopia aidha imetangaza kuwa Addis Ababa inapinga pendekezo la Misri la kuweko mpatanishi katika mazungumzo hayo na kuishutumu Cairo kuwa inafanya njama ya kufelisha yale yote yaliyoafikiwa huko nyuma na pande tatu za Ethiopia, Sudan na Misri yaliyotiwa saini mwaka 2015 kuhusu haki ya kutumia maji ya Mto Nile kiuadilifu.
Televisheni hiyo ya taifa ya Ethiopia vile vile imesema kuwa nchi hiyo imeheshimu vipengee vyote vya jinsi ya kutumia kiuadilifu maji ya Mto Nile bila ya kuziletea madhara nchi nyingine zinazopakana na mto huo.
Itakumbukwa kuwa, jana na Wizara ya Maji na Kilimo cha Unyunyizaji ya Misri ilitoa taarifa baada ya mazungumzo ya pande tatu za Ethiopia, Misri na Sudan mjini Khartoum na kusema kuwa, "Mazungumzo yamevunjika kutokana na ukwamishaji mambo wa Ethiopia."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Cairo inakaribisha kwa mikono miwili upatanishi wa kimataifa, baada ya duru kadhaa za mazungumzo ya pande mbili kutozaa matunda.
Hata hivyo madai hayo yamepingwa na Ethiopia na kusema kuwa, kilichokwamisha mazungumzo hayo ni njama za Misri za kukwepa kutekeleza makubaliano ya mwaka 2015 kati ya pande hizo tatu na njama zake za kutaka kuingiza upande wa nne hasa Marekani kwenye mazungumzo hayo.