Velayati: Uhusiano wa Iran na China ni wa kistratejia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56801-velayati_uhusiano_wa_iran_na_china_ni_wa_kistratejia
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Anayehusika na Masuala ya Kimataifa amesema kuwa uhusiano wa siku zote wa Iran na China ni wa kistratejia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 23, 2019 04:34 UTC
  • Velayati: Uhusiano wa Iran na China ni wa kistratejia

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Anayehusika na Masuala ya Kimataifa amesema kuwa uhusiano wa siku zote wa Iran na China ni wa kistratejia.

Dakta Ali Akbar Velayati amekutana na kufanya mazungumzo hapa Tehran na Mjumbe Maalumu wa China katika Masuala ya Mashariki ya Kati na kuitaja misimamo ya China kuhusu Iran kuwa ni chanya. Dakta Velayati ameongeza kuwa China ni nchi muhimu kwa Iran na siku zote kumekuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya nchi mbili hizi. 

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Anayehusika na Masuala ya Kimataifa ameashiria pia namna Syria miaka minane iliyopita ilivyokabiliwa na hujuma za nchi ajinabi na magaidi wanaoungwa mkono na nchi hizo na kueleza kuwa: Tangu awali Iran imeiunga mkono nchi rafiki na ndugu ya Syria na suala hilo limejiri kwa Iraq pia. Amesema, Baghda ingeangukia mikononi mwa magaidi kama isingekuwa misaada ya Iran. 

Vita nchini Syria
 

Dakta Ali Kbar Velayati ameashiria pia hujuma na vita huko Yemen na kueleza kuwa mustakbali wa eneo uko wazi sana na bila shaka Syria, Yemen na Iraq zitaibuka na ushindi na amani kurejea katika eneo. 

Katika mazungumzo hayo naye Zhai Jun Mjumbe Maalumu wa China katika Masuala ya Mashariki ya Kati ameshukuru ushirikiano chanya wa Iran katika eneo na kueleza kuwa: Uhusiano wa Iran na China upo katika hali nzuri sana na ushiriki wa kistratejia wa nchi mbili umepiga hatua kubwa.