Zarif: Wairani hawatasalimu amri mbele dhulma za Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia vikwazo vipya vya Marekkani dhidi ya Iran na kusema kuwa, hata kama Marekani itawawekea vikwazo wanaume, wanawake na watoto wote wa Iran kamwe Wairani hawatasalimu amri na kupiga magoti mbele ya serikali ya Washington.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa: Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya wafanyakazi wa sekta ya ujenzi nchini Iran ni kielelezo cha kufeli sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa za serikali ya Washington.
Alkhamisi ya wiki hii Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliweka vikwazo vipya dhidi ya sekta ya ujenzi na mada zinazohusiana na shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran.
Zarif amesema kuwa, badala ya kuendelea kujitia mashakani, Marekani inapaswa kutupilia mbali siasa zake zilizofeli na kurejea kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Mwezi Mei mwaka 2018 Rais Donald Trump wa Marekani alichukua uamuzi usio wa kisheria na kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1.
Iran nayo mwezi Mei mwaka huu wa 2019 ilichukua uamuzi wa kupunguza utekelezaji wa vipengee vya makubaliano hayo baada ya wanachama wa JCPOA kutotekeleza majukumu yao.