Maandamano ya tarehe 13 Aban yafanyika kote Iran ya Kiislamu
Marasimu ya maandamano ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa yamefanyika mapema leo hapa Tehran sambamba na miji mingine ya Iran kwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo wanachuo na viongozi wa serikali.
Leo Jumatatu tarehe 13 mwezi Aban kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ambayo ni sawa na tarehe Nne Novemba 2019 miladia inatambulika hapa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa. Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 13 mwezi Aban mwaka 1358 Hijria Shamsia sawa na Novemba Nne mwaka 1979 wanachuo wa Iran waliliteka pango la ujasusi la ubalozi wa Marekani hapa Tehran kulalamikia njama mbalimbali zilizokuwa zikitekelezwa na Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Shirika la Habari la Iran limeripoti kuwa, washiriki wa maandamano ya leo ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Kupambana na Ubeberu wa Dunia wamepiga nara za "Mauti kwa Marekani na Mauti kwa Israel" na kutangaza hasira na ghadhabu zao dhidi ya Uistikbari wa Kimataifa. Wapiga picha na waandishi habari wa Kiirani zaidi ya 2500 na wale wa kigeni zaidi ya 150 wamehudhuria maadhimisho ya leo ya tarehe 13 Aban.