Kamanda Mkuu wa IRGC: Tutavigeuza vitisho vya adui kuwa fursa
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amewahutubu maadui wa taifa la Iran kwa kusema: 'Tutageuza kila vitisho mnavyovianzisha kuwa fursa na kusambaratisha kila lengo mnalofuatilia.
Meja Jenerali Hussein Salami, ameyasema hayo leo Alkhamisi akiashiria mwendelezo wa hatua za maadui dhidi ya taifa la Iran na kubainisha kwamba: "Tumejifunza kwamba ni lazima tushinde, na kwa kuwa na vijana wanamapambano kamwe hatuwezi kushindwa." Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza kwamba katika vita vya kiuchumi na operesheni za kisaikolojia adui amefahamu azma, msimamo imara na ghera ya raia wa nchi hii.
Kwa mujibu wa Meja Jenerali Hussein Salami raia wa Iran pia wataibuka washindi katika vita hivi vya kiuchumi. Wakati huo huo Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kwamba, haki za kisheria na maslahi ya wananchi wa Iran, ni mambo yasiyokubali kufanyiwa muamala, na kwamba iwapo Marekani na nchi za Ulaya zitaendelea kujaribu kuirejesha nyuma nchi hii basi hazitofikia malengo yao ghairi ya kukatishwa tamaa.