"Ni fedheha kwa Marekani kuwaunga mkono Wairani wanaofanya fujo"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57362
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ni fedheha kwa Marekani kutangaza wazi wazi kuwa inawaunga mkono wanaofanya fujo na kuzusha ghasia kwa kisingizio cha kulalamikia ongezeko la bei ya petroli hapa nchini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 19, 2019 08:09 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ni fedheha kwa Marekani kutangaza wazi wazi kuwa inawaunga mkono wanaofanya fujo na kuzusha ghasia kwa kisingizio cha kulalamikia ongezeko la bei ya petroli hapa nchini.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo na kuongeza kuwa, utawala wa Washington ambao umelisakama taifa la Iran kwa ugaidi wa kiuchumi haustahiki kudai kuwa unawaunga mkono wananchi wa Iran.

Amebainisha kuwa, "Utawala ambao unachukua hatua za kulibana kiuchumi taifa hili na hata kuzuia kuingizwa nchini chakula na dawa zinazohitajika na wakongwe na wagonjwa hauwezi kudai kuwa uko pamoja na Wairani. Mike Pompeo anapaswa kutoa maelezo kwanza kuhusu ugaidi wa kiuchumi na jinai dhidi ya binadamu ambazo utawala wa Washington unawafanyia wananchi wa Iran."

Kadhalika Dakta Zarif amezionya nchi za Ulaya dhidi ya kuwaunga mkono wafanya fujo katika maandamano ya amani ya Wairani wanaolalamikia kupanda kwa bei ya petroli.

Serikali ya Iran imekata ruzuku ya mafuta, hatua iliyosababisha kupanda bei ya petroli nchini

Amesema, "Mataifa ambayo yanajificha nyuma ya mapungufu yao na kufeli kwao kusimama dhidi ya hatua ghalati za Marekani yatabeba dhima ya vitendo vyao hivyo hatari."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema matamshi ya maafisa wa serikali ya Washington kuwa wako pamoja na wananchi wa Iran ni hadaa, urongo unaoaibisha na upotoshaji wa kupindukia.