Jahangiri: Iran itatoa jibu kali kwa nchi zinazoingilia mambo yake ya ndani
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadahrisha kuwa: "Iwpao itathibiti kuwa nchi za eneo zimehusika katika ghasia na machafuko ya hivi karibnu nchini Iran, basi bila shaka zitapokea jibu kali."
Ishaq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran ameyasema hayo leo Jumamosi na kuongeza kuwa: "Nchi za eneo zinapaswa kuamiliana na Iran kwa adabu na heshima la sivyo zitapokea jibu kali."
Jahangiri ameashiria namna ambavyo, Marekani ilikusudia kuuangamiza uchumi wa Iran kupitia vikwazo lakini haikufanikiwa na sasa imeamua kuibua ghasia na machafuko ili kutoa pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu lakini haitafanikiwa katika hilo pia.
Itakumbukwa kuwa, Ijumaa wiki iliyopita, serikali ya Iran iliamua kukata ruzuku ya mafuta iliyokuwa ikiitoa.

Pamoja na kuondolewa ruzuku hiyo, bado Iran ni miongoni mwa nchi ambazo bei ya mafuta ya petrol ni ya chini zaidi duniani ambapo kwa sasa lita moja ya petroli kwa watumizi wa kawaida ni takribani senti 14 za Kimarekani. Maandamano ya kulalamikia hatua hiyo yalitumiwa vibaya na wahuni ambao waliibua ghasia na machafuko. Katika siku za hivi karibuni wananchi wa Iran wameandamna kulaani ghasia hizo.
Msemaji wa Vyombo vya Mahakama vya Iran Gholma-Hossein Esmaili amesema maafisa wa usalama wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wamefanikiwa kuwakamata vinara 100 waliokuwa wakiongoza ghasia na machafuko kote Iran.