Mtaalamu wa kisiasa Uturuki: Wairan wamezishinda Marekani na utawala haramu wa Israel
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa nchini Uturuki amesema kuwa, hatua ya kuwadhibiti wafanya ghasia na vurugu nchini Iran imefelisha njama za Marekani na utawala haramu wa Israel.
Rahmatullah Sharifi ameyasema hayo katika mahojiano na Redio Tehran akiwa mjini Istanbul na kuongeza kwamba, baada ya uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Iran kuondoa ruzuku ya mafuta, kundi fulani la wapinzani wa mfumo wa Kiislamu na kupitia uungaji mkono na uchochezi wa Marekani na utawala haramu wa Kizayuni, lilipotosha matakwa halali ya wananchi kwa kuibua ghasia na machafuko. Ameendelea kubainisha kwamba hata hivyo kundi hilo lilidhibitiwa na maafisa usalama ambapo mamia kati yao walitiwa mbaroni.
Rahmatullah Sharifi ameashiria pia uchochezi wa vyombo vya habari vya madola ya Magharibi kuhusiana na suala hilo na kusema kuwa katika miaka ya hivi karibuni nchi za Magharibi zimekuwa zikitumia vyombo vya habari kama wenzo na silaha ya ukoloni ambapo kwa kukuza na kupindisha ukweli wa mambo, huweza kuzipotosha fikra za walio wengi dhidi ya nchi zilizo huru na kujitegemea. Kufuatia ghasia za wiki iliyopita hapa nchini Iran, mamilioni ya Wairani wamekuwa wakifanya maandamano makubwa katika miji tofauti ya nchi hii kuwalaani wafanya ghasia hao wanaoungwa mkono na Marekani, utawala wa Kizayuni na baadhi ya tawala tegemezi za kieneo.