Watu 789 wajiandikisha kuwania ubunge Iran katika siku ya kwanza ya usajili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57627-watu_789_wajiandikisha_kuwania_ubunge_iran_katika_siku_ya_kwanza_ya_usajili
Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran amesema: "Katika siku ya kwanza ya kujiandikisha wagombea katika awamu ya 11 Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, watu 789 wamejisajili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2019 03:53 UTC
  • Watu 789 wajiandikisha kuwania ubunge Iran katika siku ya kwanza ya usajili

Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran amesema: "Katika siku ya kwanza ya kujiandikisha wagombea katika awamu ya 11 Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, watu 789 wamejisajili.

Sayyid Ismail Mousavi, Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi Katika Wizara ya Mambo ya Ndani ameongeza kuwa: "Kati ya watu hao 726, asilimia 92 walikuwa ni wanaume na asilimia nane wanawake."  Ameongeza kuwa mkoa wa Tehran ndio uliokuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliojiandikisha ambapo wagombea 221 wamewasilisha majina yao.

Zoezi la uandikishaji wagombea wa uchaguzi wa awamu ya 11 Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, lilianza rasmi Jumapili.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Abdul Ridha Rahmani Fazli alizindua zoezi hilo la uandikishaji  wa wale wanaotaka kugombea ubunge ambapo mbali na kujiandikisha katika Makao Makuu ya Uchaguzi mjini Tehran, pia wanaweza kujiandikisha katika ofisi za wakuu wa mikoa kote nchini.

Wanaokusudia kushiriki katika uchaguzi wa Bunge la Iran wana hadi 7 Disemba kujiandikisha.

Bunge la Iran

Baaada ya kumalizika mchakato wa kujiandikisha, Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani yatatoa tangazo la kuanza rasmi kampeni za uchaguzi Februari 13. Uchaguzi wa Bunge la Iran umepangwa kufanyika Februari 21 katika maeneo bunge 208 kote Iran kwa ajili ya kuwachagua wabunge 290.

Aidha katika siku hiyo pia kutafanyika uchaguzi mdogo wa baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu katika majimbo ya Tehran, Fars, Khorassan Kaskazini, Khorassan Ravazi na Qum.