Iran yazialika nchi za eneo kushiriki katika mazoezi ya kijeshi baharini
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kufanyika mazoezi ya pamoja ya majeshi ya majini ya Iran, China na Russia na kusema Iran inazialika nchi zote za eneo kushiriki katika mazeozo yajayo ya majeshi ya majini.
Admeli Hussein Khanzadi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumapili wakati akizungumza na waandishi habari pembizoni mwa mazoezi ya pamoja ya majeshi ya majini ya Iran, Russia na China na kuongeza kuwa, hadi sasa mazoezi hayo yaliyoanza Ijumaa yanaendelea kwa mafanikio. Amebaini kuwa: "Iran inataka kuzisaidia nchi za eneo la Asia Magharibi ili usalama wa eneo upatikane kwa msaada na ushirikiano wa nchi za eneo."
Admeli Khanzadi amesema katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, adui amekuwa akiiwekea Iran vikwazo na kujaribu kutumia njia hiyo kuitenga Iran lakini si tu kuwa vikwazo hivyo havijaweza kufanikiwa, bali vimepelekea kuwepo mshikamano na ushirikiano zaidi baina ya madola makubwa kieneo.
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, leo zile zama za Marekani kutamba katika eneo zimefika ukingoni na kwa msingi huo Wamarekani wanapaswa kuondoka katika eneo la Asia Magharibi.
Mazoezi ya Kijeshi ya Iran, Russia na China yalianza Ijumaa 27 Disemba na yataendelea kwa muda wa siku nne katika eneo lenye umuhimu wa kistratijia la kaskazini mwa Bahari ya Hindi na Bahari ya Oman.
Kati ya malengo ya mazoezi hayo ni kubadilishana uzoefu baina ya nchi tatu na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na ugaidi na uharamia.