Kamanda wa IRGC: Tutalipiza kisasi cha kuuawa shahidi Jenerali Soleimani
(last modified Tue, 07 Jan 2020 08:16:07 GMT )
Jan 07, 2020 08:16 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Tutalipiza kisasi cha kuuawa shahidi Jenerali Soleimani

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kisasi cha taifa la Iran kwa damu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha SEPAH kitakuwa kikali, madhubuti, cha kutisha na kamilifu.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema hayo leo mjini Kerman, kusini mashariki mwa nchi anakozikwa Haji Soleimani ambapo pia amejumuika na familia, ndugu, marafiki na wakazi wa mji huo katika kuuaga mwili wa shahidi huyo aliyeuawa kikatili na Marekani.

Meja Jenerali Salami ameeleza bayana kuwa, "Luteni Jenerali Qassem Soleimani alivaa magwanda ya kijeshi kwa miaka 41 na alifahamu vyema kuwa, amevaa vazi hilo kwa sababu ya izza na heshima ya Uislamu."
Ameongeza kuwa, shakhsia ya Jenerali Soleimani inavuka mipaka ya Iran, na ulimwengu wa Kiislamu umemfanya kuwa shakhsia anayependwa na kusifiwa na wanadamu wote, na kumuona kama kiigizo chema katika mapambano dhidi ya dhulma.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Bila shaka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu litachukua hatua kali ya kulipiza kisasi na Marekani itajuta."

Maelfu ya Wairani wakiwaaga mashahidi wa Baghdad

Malaki ya wananchi wa Iran wamekusanyika mjini Kerman kwa ajili ya kuiaga miili ya Jenerali Soleimani pamoja na Meja Janerali Hossein Pourjafari, ambaye pia aliuawa shahidi katika shambulizi hilo la kigaidi la Marekani.

Takriban Wairani milioni saba walikusanyika jana katika mji mkuu wa Iran, Tehran kuuaga mwili wa Jenerali Soleimani pamoja na mashahidi wenzake kabla ya kuelekea katika mji mtakatifu wa Qum. Matembezi ya kumuomboleza na kumuenzi Haji Soleimani na mashahidi wenzake yalifanyika pia katika miji ya Baghdad, Karbala, Najaf, Ahwaz na Mashhad.