Shamkhani: Kuondoka Marekani katika eneo kunapasa kuwa kipaumbele
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58489-shamkhani_kuondoka_marekani_katika_eneo_kunapasa_kuwa_kipaumbele
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa kuondoka Marekani katika eneo kunapasa kuwa kipaumbele na kueleza kuwa hakuna siku eneo la Asia Magharibi litakuwa na amani ya kudumu madhali wangalipo wanajeshi magaidi wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 13, 2020 09:06 UTC
  • Shamkhani: Kuondoka Marekani katika eneo kunapasa kuwa kipaumbele

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa kuondoka Marekani katika eneo kunapasa kuwa kipaumbele na kueleza kuwa hakuna siku eneo la Asia Magharibi litakuwa na amani ya kudumu madhali wangalipo wanajeshi magaidi wa Marekani.

Ali Shamkhani Jumatatu hii amekutana na kufanya mazungumzo hapa Tehran na Imad Khamis Waziri Mkuu wa Syria na huku akisisitiza suala la kuwa kitu kimoja nchi za eneo na kwamba kuondoka shari ya Marekani katika eneo kunakaribia, ameongeza kuwa Iran kwa kuvurumisha makombora katika kambi ya Marekani ya Ain al Asad na kutoa jibu kali kwa jinai za Marekani kwa mara nyingine tena imethibitisha kuwa haitasalimu amri na kukaa kimya kuhusu suala la kulinda amani na maslahi ya taifa hili.  

Ali Shamkhani katika mazungumzo na Imad Khamis, Waziri Mkuu wa Syria hapa Tehran 

Shamkhani amesema kuwa Rais wa Marekani na washauri wake wapumbavu walidhani kwamba kwa kumuua kigaidi Luteni Jenerali shahidi  Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) wanaweza kusambaratisha muhimili wa muqawama katika eneo. Ameongeza kuwa damu ya Luteni Jenerali Shahidi Soleimani na wanajihadi wenzake imezidisha umoja na kuimarisha zaidi muhimili wa muqawama na chuki ya watu wa eneo na ulimwenguni dhidi ya Marekani. 

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametangaza pia kuunga mkono hatua zinazotekelezwa na serikali ya Syria kwa ajili ya kuhitimisha uwepo wa makundi ya kigaidi nchini humo na kueleza kuwa wizi wa mafuta unaofanywa Syria na uporaji wa maliasili za nchi hiyo ni maafa mengine ambayo yanaweza kufikia ukomo kwa kuondoka kikamilifu Marekani katika eneo. 

Katika mazungumzo hayo, Imad Khamis Waziri Mkuu wa Syria amepongeza jitihada kubwa na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Syria katika vita dhidi ya ugaidi na kueleza kuwa lengo la Luteni Jenerali Soleimani lilikuwa ni kuwalinda raia waliodhulumika mbele ya udhalimu na ukandamizaji wa Marekani, utawala wa Kizayuni na mfumo wa uistikbari. Waziri Mkuu wa Syria ameongeza kuwa uhhusiano wa Tehran na Damascus unapasa kustawishwa zaidi na zaidi kwa kupanuliwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi mbili.