Zarif: Magharibi inapaswa iache kuwapa hifadhi na kuwasaidia kifedha magaidi
(last modified Sun, 02 Aug 2020 03:30:15 GMT )
Aug 02, 2020 03:30 UTC
  • Zarif: Magharibi inapaswa iache kuwapa hifadhi na kuwasaidia kifedha magaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia ulazima wa nchi za Magharibi kuacha kuyahami na kuyaunga mkono magenge ya kigaidi yanayopinga Mapinduzi na akasema: Kutokea kwenye maficho yao walikopewa hifadhi ndani ya Marekani na Ulaya, magaidi wanaandaa machafuko na mauaji ya raia wa Iran.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo kufuatia kukamatwa na kikosi cha usalama wa taifa kinara mmoja wa genge la kigaidi na linalopinga Mapinduzi.

Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Zarif ameashiria uungaji mkono wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, kwa magaidi wenye nia ovu ya kuipiga vita na kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu na akasema: "Magharibi inapaswa iache kuwapa hifadhi na kuwasaidia kifedha magaidi."

Amefafanua kuwa: "Magaidi wanaeneza chuki kutokea kwenye maficho yao ndani ya Marekani na Ulaya, wanapanga na kuchochea mauaji na machafuko na wanakiri pasi na kuona aibu kuwa ndio wanaohusika na mauaji ya raia wasio na hatia wa Iran."

Jamshid Sharmahd, kinara wa genge la kigaidi la Tondar lenye makao yake nchini Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amehitimisha ujumbe wake huo kwa kuashiria hatua za nchi za Magharibi za kujaribu kusafisha sura chafu za magenge ya kigaidi yanayojaribu kufanya vitendo vya hujuma ndani ya Iran na akasema:"Hila na udanganyifu haviwezi kuficha uzandiki huo."

Wizara ya Usalama ya Iran jana ilitoa taarifa na kueleza kwamba vikosi vya usalama vimetekeleza operesheni tata na kabambe na kufanikiwa kumtia nguvuni Jamshid Sharmahd, kinara wa kundi la kigaidi la Tondar, aliyekuwa akiongoza operesheni za mtutu wa bunduki na hujuma ndani ya Iran kutokea mafichoni kwake nchini Marekani.../