Dec 18, 2020 04:02 UTC
  • Zarif: Vikwazo vya Washington vimewadhuru Wamarekani wenyewe

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera ya vikwazo ya Washington imekuwa na madhara makubwa hata kwa wananchi wa Marekani wenyewe na kampuni zao na hivyo kusababisha ukosefu wa ajira miongoni mwa Wamarekani.

Muhamamd Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo amemhutubu mwenzake wa Marekani, Mike Pompeo kwa kumuambia: Vizingiti vyenu wenyewe vimezifungia kampuni za Marekani nje ya soko la Iran lenye maliasili na rasimali watu.

Huku akiitaja sera ya mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani kama kufeli kwa hali ya juu zaidi, Dakta Zarif amebainisha kuwa, sera hiyo si tu ilipelekea kufutwa kwa mkataba wa mauzo ya ndege 88 za abiria za shirika la Boeing la US kwa Iran, lakini pia ilisababisha kupotea kwa nafasi za ajira kwa Wamarekani.

Kauli ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ni radiamali kwa ujumbe wa hivi karibuni wa Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeondoka aliyetangaza katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu vikwazo vipya vya Washington dhidi ya taifa la Iran.

Vikwazo vilivyofeli vya US dhidi ya Iran

Kabla ya hapo, Dakta Zarif alisema iwapo rais mteule wa Marekani, Joe Biden anataka kuirejesha nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, sharti atekeleza wajibu wa US katika mapatano hayo na afute vikwazo (vya kidhalimu dhidi ya Iran).

Amesema rais anayeondoka wa Marekani, Donald Trump na washirika wake wanaondoka mikono mitupu kwani hawajastafidi na chochote kwa kuiondoa nchi hiyo kinyume cha sheria katika mapatano hayo ya kimataifa.

 

Tags