Iran: Waliovunja ahadi wanapaswa kufanya maamuzi magumu
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema wale ambao walivunja ahadi zao ndio wanaopaswa kubainisha iradi yao ya kisiasa na ndio wanaopaswa kuchukua maamuzi magumu.
Majid Takht-Ravanchi alisema hayo jana kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa, kinyume na washiriki wengine wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambao kazi yao kubwa ndani ya miaka kadhaa iliyopita imekuwa kubwabwaja tu, lakini Jamhuri ya Kiislamu ndiyo nchi pekee ambayo imelipa gharama kubwa kuyalinda mapatano hayo ya kimataifa.
Amesema Iran imeonesha muamana wake katika kipindi chote cha mazungumzo ya JCPOA hadi yalipofikia tamati, na hata wakati wa utekelezwaji wake, licha ya kuwa taifa hili halijastafidi na mapatano hayo kama ilivyostahili, kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema nchi ambazo zilivunja ahadi zao, yaani Marekani na nchi tatu za Ulaya (Ujerumani, Uingereza na Ufaransa) ndizo zinazopaswa kuonesha uaminifu na irada yao ya kisiasa. Amesisitiza kuwa, nchi hizo zinapaswa kuchukua maamuzi magumu wakati huu ambapo mazungumzo ya JCPOA yanaendelea kwa mwendo wa kinyonga.
Takht-Ravanchi ameeleza bayana kuwa, Marekani inapaswa kutoa dhamana na hakikisho kuwa haitajiondoa tena kwenye JCPOA, kwa kuwa ilijiondoa kinyume cha sheria katika makubaliano hayo bila sababu yoyote ya msingi wala mantiki.
Hivi karibuni pia, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeongoza timu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna alisisitiza kuwa, sasa ni wakati wa pande nyingine husika ndani ya mapatano ya JCPOA kuchukua maamuzi, na kwamba nchi hizo zinapasa kuchukua maamuzi magumu.