Jul 03, 2021 12:41 UTC
  • Rouhani: Marekani iwajibishwe kwa kutungua ndege ya abiria ya Iran

Rais Hassan Rouhani wa Iran ameikosoa vikali Marekani kwa kutoomba radhi kwa kushambulia ndege ya abiria ya Jamhuri ya Kiislamu mwaka 1988 katika Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kuwa, Washington inapaswa kubebeshwa dhima kwa kuwaunga mkono waliotenda jinai hiyo.

Akihutubia Jopokazi la Kupambana na Corona leo Jumamosi hapa mjini Tehran, Rais Rouhani ameeleza kusikitishwa kwake namna Marekani haijawahi kuomba radhi rasmi tokea wakati huo hadi sasa kwa ukatili huo, bali hata ilimtunuku nishani kamanda wa Jeshi la Majini la nchi hiyo aliyetekeleza hujuma hiyo.

Dakta Rouhani amekitaja kitendo hicho cha Wamarekani kuwa cha kutisha, kuogofya na kisichokubalika, huku akisisitiza kuwa utawala wa Washington unapaswa kubaini na kukumbuka kuwa ulitenda jinai kubwa mwaka 1988.

Wananchi wa Iran hii leo wameadhimisha miaka 33 tokea ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran Air iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa Iran kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, iliposhambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi.

Makamanda wa jeshi, maafisa wa serikali na wananchi wa Iran katika kumbukizi ya kushambuliwa 'Airbus'

Wananchi wa Iran zikiwemo familia za wahanga wa ukatili huo wamekusanyika katika eneo la Hormuzgan kwa ajili ya kumbukumbu ya umwagaji damu huo, huku wakipiga nara za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Israel.'

Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama na ugaidi wa serikali ya Marekani. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.

Tags